IDARA YA MAJI MAKETE YAENDELEA NA UKARABATI WA CHANZO CHA MAJI KIJIJI CHA IVALALILA

Saturday, November 16, 20130 comments

Zoezi la kufanya ukarabati mkubwa katika chanzo cha maji cha Kidwiva kilichopo katika kijiji cha Ivalalila wilaya ya Makete mkoa wa Njombe lililotarajiwa kumalizika leo, limeshindwa kumalizika kama ilivyotarajiwa

Kauli hiyo imetolewa na meneja wa mamlaka ya maji makete mjini Bw. Yonas Ndomba wakati akizungumza na mtandao huu kuhusu maendeleo ya ukarabati huo ambao umesababisha ongezeko la mgawo wa maji Makete mjini

Meneja Ndomba amesema walitarajia zoezi hilo likamilike jana au leo Ijumaa lakini kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwenye chanzo hicho kwa siku tatu mfululizo kumepelekea mafundi hao kukwama kuendelea na ukarabati huo

Amesema wanatarajia kuendelea na zoezi hilo hapo kesho Jumamosi kama mvua hazitanyesha wanategemea kumaliza ukarabati huo na hali ya maji kwa wananchi wa Makete mjini itarejea kama kawaida
Amewaomba wananchi hasa wateja wa maji kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha matengenezo kwani wanajitahidi kukamilisha ukarabati huo

Wakati huo huo Meneja huyo amesema mabomba ya maji kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji katika chanzo hicho tayari yamewasili katika kijiji cha Ivalalila na kinachosubiriwa na ukaguzi wa mabomba hayo kama yana viwango vinavyotakiwa na serikali

Amesma endapo ukaguzi huo utaonesha kama yana viwango stahili wataendelea na uboreshaji wa miundombinu hiyo
 
NA EDWIN MOSHI
Share this article :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. MAKETE BLOG - All Rights Reserved
Designed by Edwin Moshi
Property of Makete District Council