KAMPENI YA TOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VVU KUTOKA KWA MAMA KWENDA KWA MTOTO MIKOA YA NJOMBE NA IRINGA YAZINDULIWA

Saturday, November 16, 20130 comments

 Kikundi cha ngoma cha WANGAMA kikitumbuiza kwenye uzinduzi huo.
 Katibu tawala mkoa wa Njombe Mgeni Baruani (kulia) akipata maelezo kwenye kituo cha afya Makambako baada ya uzinduzi huo
Jamii imeshauriwa kuwahimiza akina mama wajawazito kuenda kwenye vituo vya huduma za afya mapema ili kuchunguzwa afya zao na endapo watabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI wataanzishiwa dawa za kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto

Rai hiyo imetolewa na katibu tawala mkoa wa Njombe Bi. Mgeni Baruani kwenye uzinduzi wa kampeni ya tokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto uzinduzi katika kituo cha afya Makambako mkoani Njombe

Bi. Baruani amesema dawa hizo za kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi toka kwa mama kwenda kwa mtoto zinatolewa bure kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Njombe na Iringa hivyo kuitaka jamii kushirikaina na serikali kuokoa maisha ya kina mama wajawazito na watoto wao watarajiwa

Pia amehimiza viongozi wote na vyombo vya habari kuongeza nguvu ya kuwahimiza wananchi wajitokeze kupima afya zao kwani bado anaamini kwa dhati kuwa Tanzania bila UKIMWI inawezekana

"Wito wangu kwa wenzi shirikianeni kuwakinga dhidi ya maambukizi watoto wenu.kwa kiongozi nawaombeni wote kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa muwe mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya vvu hususan kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwani pia ni jukumu la kila mmoja wetu kwenye jamii kuhakikisha kuwa tunawanusuru watoto na maambukizi haya" alisema Mgeni

Awali akisoma taarifa ya uzinduzi huo mratibu wa UKIMWI halmashauri ya mji wa Makambako Bi. Magdaleth Msasi amesema mpango huo utafuatwa vizuri ni dhahiri kuwa kuna mafanikio katika kupunguza maambukizi ya vvu toka kwa mama kwenda kwa mtoto katika mkoa wa Njombe na Iringa

Aidha alisema ni vyema kina mama wajawazito kuendelea kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ya uzazi na mtoto chini ya usimamizi wa mhudumu wa afya kwani itamhakikishia kujifungua kwa usalama vilevile kupewa elimu ya namna ya kuzuia maambukizi kwa mtoto anayetarajiwa kuzaliwa na ambaye amezaliwa tayari

Mpango huo uliozinduliwa kwa mikoa ya Njombe na Iringa unalenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 50 miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuzaa (15-49) na pia kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango miongoni mwa akina mama wanaoishi na VVU.
Habari/picha na Veronica Mtauka,www.edwinmoshi.com, Makambako.
Share this article :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. MAKETE BLOG - All Rights Reserved
Designed by Edwin Moshi
Property of Makete District Council