JELA MIAKA MIWILI KWA KUMGONGA NA KUMUUA DEREVA BODABODA MAKETE

Thursday, November 07, 20130 comments


Mahakama ya wilaya Makete mkoani Njombe imemkuata na hatia ya makosa matatu Bw. Mdula Abdula mwenye umri 43 kwa matumizi mabaya ya barabara hali iliyopelekea kusababisha kifo, hasara ya gari na pikipiki baada ya kushindwa kulimudu gari alilokuwa anaendesha na kumhukumu kwenda jela miaka miwili ama kulipa faini ya shilingi 90,000/=.

Akisoma shitaka hilo mwendesha mashtaka wa polisi Bw. Gozbert Komba mbele ya hakimu mkazi (w) amesema mnamo Agosti 30 mwaka huu mshitakiwa alishindwa kulimudu gari lenye namba za usajili T 872 CJQ kutokana na mwendo kasi na kugonga pikipiki yenye namba za usajili T 225 BGE aina ya SUNLG na kumsababishia kifo cha Haruni Yahamusi aliyekuwa dereva wa pikipiki hiyo.

Ameongeza kuwa gari hilo lilikuwa linatokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam na kusababisa ajali katika kijiji cha Kimani kilichopo kata ya Mfumbi wilayani Makete majira ya saa nne na nusu asubuhi.

Akisoma hukumu mahakamani hapo hakimu amesema amemeridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mtuhumiwa kukiri kutenda kosa hilo hivyo kumhukumu kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi elfu tisini pamoja na kufungiwa leseni ya udereva kwa muda wa miezi miwili, hii ni kutokana na sheria za nchi, na pia mshitakiwa ni kosa lake la kwanza.

Aidha mshitakiwa huyo Bwana Abdala amekubali kulipa faini ya shilingi 90 kwa mahakama hivyo kuwa huru na leseni yake kuzuiliwa na ataipewa baada ya miezi miwili kupita

Wakati huo huo kesi inayomkabili aliyewahi kuwa askari polisi kituo cha polisi Makete PC Joseph Gerevaz anaye tuhumiwa kwa kosa la mauaji ya mwalimu wa shule ya sekondari ya Kitulo marehemu Sote Kawamba imearishwa kwa mara nyingine tena katika mahakama ya wilaya hadi Novemba 8 mwaka huu

Na:Henrick Idawa
Share this article :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. MAKETE BLOG - All Rights Reserved
Designed by Edwin Moshi
Property of Makete District Council