HALMASHAURI YA WILAYA YA MAKETE YAKATAA KUPOKEA MRADI WA MAJI AMBAO HAUJARIDHIKA NAO

Saturday, November 16, 20130 comments

 Mradi wa maji uliopo Matamba.
=====
Kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya maji na mingine kujengwa chini ya kiwango kumeonekana kuwa mwiba mchungu kwa wananchi na baadhi ya viongozi wapenda maendeleo wilayani Makete mkoani Njombe

Hayo yamebainika hii leo kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Makete wilayani hapo

Akizungumza kwenye kikao hicho, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka amesema kwa upande wa tarafa ya Matamba amesema yeye kama mtia saini mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo hataipokea mpaka akatapofanya ukaguzi hatua kwa hatua

"Mimi nitakwenda Matamba na kuwafuata wananchi tunakwenda hatua kwa hatua na kuzungumza nao wakati wa ukaguzi na wakiridhika na ujenzi huo wa mradi, mimi nitaupokea wakikataa sitaupokea" alisema Okoka

Amesema kwa kiasi kikubwa anashangazwa na baadhi ya viongozi wa Matamba ambao hakuwataja kumwambia kuwa hana mamlaka ya kufanya mikutano kwenye maeneo hayo, na kufafanua kuwa yeye kama mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete ana uwezo wa kufanya mikutano sehemu yeyote ile ndani ya wilaya yake bila kizuizi, na hivyo viongozi hao wasimkwamishe

Akichangia hoja hiyo, katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu amesema ni aibu kwa viongozi pindi miradi ya maji inapoonekana kutokamilika ilihali taarifa zinazotolewa zinaonesha kuwa miradi hiyo imefanyika na imekamilika 

Akizungumzia mradi wa Matamba amesema hali ni mbaya kwani mradi huo hautoi maji licha ya taarifa kudai kuwa umekamilika, na kudai kuwa huu si muda wa kulumbana kumtafuta mchawi na badala yake kinachotakiwa ni maji yawafikie wananchi na si kitu kingine
Naye mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro ameagiza kuwa tatizo hilo la ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ikiwemo Matamba lifanywe haraka iwezekanavyo ukizingatia kuwa serikali imetoa kipaumbele kwa miradi hiyo ya maji
 
Na Edwin Moshi
Share this article :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. MAKETE BLOG - All Rights Reserved
Designed by Edwin Moshi
Property of Makete District Council